27 Februari 2025 - 20:08
UN: Israel inakanyaga haki za binadamu Gaza, Ukingo wa Magharibi

Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema utawala wa Israel umekuwa ukipuuza usio na kifani haki za binadamu" katika Ukanda wa Gaza, na kuitaja hali ya kibinadamu katika eneo hilo lililozingirwa kuwa "janga."

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Turk amesema hayo katika ripoti yake ya kina inayoelezea hali ya haki za binadamu huko Gaza, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel na Quds Mashariki siku ya Jumatano.

Akihutubia kikao cha 58 cha Baraza la Haki za Kibinadamu mjini Geneva kuhusu hali ya ndani ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Turk aliitaja hali ya kibinadamu ya Gaza kuwa ni janga iliyosababishwa na vizingiti na vikwazo vikali vilivyowekwa na utawala ghasibu wa Israel.

"Hakuna kinachohalalisha operesheni za kuogofya za jeshi la Israel huko Gaza, operesheni ambazo mara kwa mara zilikiuka sheria za kimataifa," Turk amesema, akiangazia uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kiraia, pamoja na nyumba, hospitali na shule huko Gaza.Ameongeza kuwa, majeshi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi yamezidisha matumizi ya "nguvu zisizo za lazima na zisizo na uwiano," na kuharibu kambi za wakimbizi, kuzuia harakati, na kuwafukuza makumi kwa maelfu ya watu kwenye makazi yao. 

Wakati huo huo, Philippe Lazzarini, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), amesema wiki kadhaa za uvamizi wa kijeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu umeligeuza eneo hilo kuwa “uwanja wa vita” na kuwaacha watu 40,000 bila makazi. 


342/